Bangi (marijuana) ni nini?
Bangi au marijuana ni dawa zinazotokana na mmea wa bangi. Kwa kawaida huvutwa au kunuswa, lakini pia inaweza kukaushwa na kuliwa.
Je, madhara ya bangi ni yapi?
Katika muda mfupi, bangi inaweza kukufanya utulie, uzungumze sana na inaweza kufanya fahamu zako zihisi kuwa na nguvu zaidi, kwa mfano, muziki unaweza kusikika ukiwa mzuri sana. Wakitumia dozi nyingi, watu wanaweza kuhisi kuugua au kupoteza fahamu, kuchanganyikiwa au wazimu. Si salama kuendesha gari baada ya kuvuta bangi. Matumizi ya muda mrefu ya bangi huweza kuathiri uwezo wako wa kujifunza na kuzingatia vitu na watumiaji wanaweza kuhisi hawana motisha au kutengwa au kupuuza mambo mengine yanayoendelea maishani mwao.
Je, madhara ya kutumia bangi katika umri mdogo ni yapi?
Watu wanaoanza kutumia bangi katika umri mdogo au wanaotumia mara kwa mara wana uwezekano mkubwa wa kupata uraibu. Hii inaweza kusababisha matatizo ya kupata usingizi, kuwashwa au kuhangaika unapoacha kutumia bangi. Ukivuta bangi pamoja na tumbaku pia utakuwa katika uwezekano mkubwa wa kupata matatizo ya kiafya yanayohusiana na uvutaji bangi, ikiwa ni pamoja na matatizo ya moyo na mapafu. Kuvuta bangi wakati wa ujauzito kunaweza pia kuathiri ukuaji wa mtoto.
Je, bangi husababisha matatizo ya afya ya akili?
Kuna uhusiano kati ya matumizi ya kawaida ya bangi na baadhi ya matatizo ya afya ya akili. Watu wanaotumia bangi mara kwa mara na kuanzia wakiwa na umri mdogo wana uwezekano mkubwa wa kukumbwa na matatizo ya hisia na njozi za uwongo. Hii ni pale ambapo wanaona au kuamini vitu ambavyo si halisi. Hatari ya madhara haya ya muda mrefu huwa makubwa iwapo mtu kwenye famili yako amewahi kuwa na matatizo ya hisia za uwongo au ugonjwa wa akili (tatizo la ugonjwa wa akili ambalo kwa kawaida huhusishwa na hali ya njozi au hisia za uwongo).
Je, madhara ya kujidunga sindano ya dawa ni yapi?
VVU, hepatitisi C na maambukizi mengine yanayohusisha damu yanaweza kusambazwa kwa kushiriki pamoja sindano na vitu vyenye ncha kali. Hii ni pamoja na kushiriki sindano ili kujidunga madawa fulani.Unapotumia sindano kujidunga madawa, kiasi fulani cha damu yako kitaingia kwenye sindano. Sindano na vitu nyenye ncha kali ambavyo mtu mwingine ametumia vinaweza kuwa na damu yenye virusi ambavyo huenda anavyo. Iwapo mnatumia kifaa kimoja cha kujidunga, unaweza kujidunga virusi kwenye damu yako. Kushiriki pamoja vifaa vingine vya kujidunga ikiwa ni pamoja na maji yaliyotumika kusafisha sindano, vijiko au vyombo vingine au vichujio, inaweza pia kuwa njia ya kuambukiza VVU na virusi vingine.
Ninawezaje kuepuka VVU ninapojidunga sindano ya dawa?
Ukijidunga madawa, epuka kushiriki pamoja vitu vyenye ncha kali, sindano au vifaa vya kujidunga. Baadhi ya maeneo hutoa sindano mpya na sehemu ya kutupa kwa usalama zile zilizotumika. Tumia maji safi yaliyochemshwa kusafisha sindano na kutupa kwa usalama vifaa vilivyotumika. Unaweza kuamua kupata matibabu kabla ya kuwa katika hatari ya VVU ili kuepuka kuambukizwa VVU. Zungumza na mhudumu wa afya, ukihitaji usaidizi kuhusu kuacha kutumia madawa.