Je, dawa ya kupunguza kiwango cha virusi kwenye damu (dolutegravir) inafanyaje kazi?
Dawa zote za kupunguza makali ya VVU hufanya kazi kwa kuzuia uwezo wa VVU wa kuzaana. Mchakato wa kuzaana kwa VVU una hatua kadhaa tofauti. Aina tofauti za dawa za kupunguza makali ya VVU huzuia VVU kuweza kukamilisha hatua tofauti katika mchakato huu. Matibabu yako yatajumuisha mchanganyiko wa dawa hizi za kupunguza makali ya VVU ambazo kwa pamoja zinaweza kufanya kiwango chako cha virusi kwenye damu kupungua na kuzuia VVU vipya kutengenezwa.
Dolutegravir ni ya aina ya dawa zinazojulikana kama dawa za kuzuia maambukizi ya VVU kwenye seli - hizi zinazuia VVU kuingiza DNA yake kwenye seli ya CD4. Bila kuwa na uwezo wa kufanya hivyo, VVU haiwezi kudhibiti seli zako za CD4.
Kwa nini dolutegravir ina kizuizi kikubwa dhidi ya usugu (dawa kutokuwa na ufanisi)?
Tunaposema kwamba dawa ina kizuizi kikubwa dhidi ya usugu, kwa kawaida tunaelezea mabadiliko kadhaa ambayo virusi vinapaswa kufanya ili dawa hiyo isiwe na ufanisi. Inaweza pia kuelezea uwezekano wa mabadiliko hayo kutokea. Kuna vipengele kadhaa kuhusu muundo wa dolutegravir (DTG) na jinsi inavyofanya kazi inayoifanya kuwa vigumu kwa VVU kuzoea na kuishinda DTG.
Mojawapo ya mambo ambayo wanasayansi huangalia ni muda ambao dawa hukaa mwilini mwako baada ya kuitumia. Ili kupima hili wanatumia kile kinachojulikana kama 'nusu ya muda' wa dawa kufanya kazi. Nusu ya muda wa dawa kufanya kazi unaelezea muda unaotumika mpaka dawa kuisha mwilini. Kuhusu DTG, dawa hii hukaa mwilini mwako kwa muda mrefu. Hii inamaanisha kuwa unaweza kufanya matibabu yako mara chache (mara moja kwa siku badala ya mara kadhaa kwa siku). Pia inamaanisha kuwa una kiwango cha juu cha ulinzi ikiwa umekosa dozi, jambo linalofanya uwezekano wa usugu wa dawa kuwa mdogo.
DTG ni dawa kali ya kupambana na VVU. Ina uwezo wa kuzuia kuenea kwa VVU kuwa katika viwango vya chini. Dawa zingine zinahitaji utumie dozi za juu ili kuwa na ufanisi.
Je, kasoro za mishipa ya neva ni nini na je, ninapaswa kuwa na wasiwasi juu yake?
Kasoro za mishipa ya neva ni aina ya tatizo la kiafya ambalo linaweza kutokea kwa watoto wakati wa hatua za awali za ujauzito. Mnamo mwaka 2018, kulikuwa na hofu kwamba wanawake walio na umri wa kuzaa hawapaswi kupewa dolutegravir baada ya utafiti mdogo uliofanyika nchini Botswana kuonyesha kuwa kutumia dolutegravir katika hatua za mwanzo za ujauzito kunaweza kuhusishwa na hatari kubwa ya kasoro za mishipa ya neva kwa watoto wachanga.
Ushahidi zaidi umepatikana unaoonyesha kwamba hatari hii ni ndogo sana kuliko ilivyofikiriwa awali. Kwa wanawake wengi, faida za kutumia dolutegravir zitazidi hatari hizi. Kwa wanawake wanaotumia kingamimba ya kuaminika ambao hawana mpango wa kupata ujauzito, madhara haya yanayoweza kutokea hayawapi wasiwasi. Lakini kwa wanawake ambao wanataka kupata watoto hivi karibuni au ambao wako katika hatua za mwanzo za ujauzito, hili linaweza kuwa jambo ambalo wanapaswa kujadili na mfanyakazi wa huduma ya afya.
Mwishowe ushauri kuhusu dolutegravir ni kwamba wanawake wanapaswa kuelewa ni zipi faida na hatari kwao na waweze kufanya maamuzi yao wenyewe kuhusu matibabu yao. Wanapaswa kuwa na uwezo wa kufikia njia za kuzuia mimba za kuaminika na chaguo mbalimbali nzuri za matibabu, ili waweze kufanya maamuzi sahihi na yenye afya ambayo yanawafaa.