Je, ugonjwa unaosababishwa na Vimelea vya Kichocho kwenye Viungo vya Uzazi vya Mwanamke (FGS) umeenea kwa kiasi gani?
Vimelea vya Kichocho (Schistosomiasis) vinapatikana sana katika maeneo ya joto na joto kiasi miongoni mwa jamii ambazo zina uwezo mdogo wa kupata maji salama au safi ya kutosha. Maambukizi ya FGS yanaweza kutokea tu wakati wanadamu wanatumia maji kutoka katika chanzo cha maji kilichochafuliwa. Ugonjwa unaosababishwa na Vimelea vya Kichocho kwenye Viungo vya Uzazi vya Mwanamke (FGS) unafikiriwa na wengi kuwa hali ya uzazi iliyopuuzwa zaidi katika nchi za Afrika zilizo ukanda wa Jangwa la Sahara. Inaathiri makumi ya mamilioni ya wasichana na wanawake katika nchi ambazo vimelea hivi vya kichocho vipo, haswa kote Afrika.
Kwa kiasi kikubwa FGS inahusishwa sana na visa vya kichocho vinavyosababishwa haswa na vimelea vya S. haematobium (mnyoo wa damu kwenye mkojo) na inakadiriwa kuwa hadi robo tatu ya wale walioambukizwa na vimelea vya S. haematobium watapata FGS, hii inatafsiriwa kuwa takriban wasichana na wanawake milioni 56. Hata hivyo licha ya jinsi ugonjwa huu unavyopatikana, kuna ufahamu mdogo sana kuhusu hali hiyo. Haujatajwa katika vitabu vingi vya matibabu na haujulikani kwa wafanyakazi wengi wa huduma ya afya.
Je, kichocho cha viungo vya uzazi kinaweza kuwaathiri wanaume?
Ndiyo. Kichocho cha viungo vya uzazi huathiri wanawake na wanaume, hata hivyo kuna utafiti zaidi na ufahamu juu ya ishara za kimatibabu na shida zinazojitokeza zenyewe kwa wanawake. Kwa wanaume huitwa Kichocho cha Viungo vya Uzazi vya Mwanaume (MGS). MGS ni ugonjwa uliopuuzwa sana na utafiti zaidi unahitajika ili kuelewa vizuri athari za kichocho cha viungo vya uzazi kwa wanaume.
Tunachojua ni kwamba dalili kwa wanaume ni pamoja na kuvimba kwa viungo vya uzazi, hali ya maumivu wakati wa uume kusimama na kumwaga, kukojoa mara kwa mara, hisia za kuungua wakati wa kukojoa, damu kwenye shahawa na tezi karibu na kibofu.
MGS inaweza kuathiri tezi za shahawa, korodani, kibofu na viungo vingine na mayai ya vimelea vya kichocho husababisha uharibifu wa tishu na kuvimba.
Kama ilivyo kwa FGS, vidonda vya viungo vya uzazi na uvimbe vinaweza kusababisha hatari kubwa ya kupata VVU.
Ni muhimu kwa wanaume kutafuta matibabu ikiwa wanafikiri wako hatarini au wana dalili za MGS. Praziquantel (PZQ) ni dawa inayotumika kutibu aina zote za ugonjwa wa kichocho, pamoja na MGS.
Je, watu wanaoishi na ugonjwa wa FGS wako katika hatari zaidi ya kupata VVU?
Kuna utafiti unaokua unaotafiti uhusiano uliopo kati ya kichocho cha viungo vya uzazi na VVU na sasa inakubalika kwa kiasi kikubwa kwamba wanawake na wasichana wanaoishi na FGS wako katika hatari zaidi ya kupata VVU. Tafiti kadhaa kubwa zimeonyesha kuwa wanawake wenye umri mkubwa walio na FGS wana uwezekano mara tatu hadi nne wa kuambukizwa VVU kuliko wanawake wasio na FGS.
Pia kuna mwingiliano mkubwa wa kijiografia wa FGS na VVU katika nchi kama vile Malawi, Msumbiji, Afrika Kusini, Tanzania na Zimbabwe. Kulingana na ushahidi huu, FGS inaweza kuonekana kama kichochezi kikubwa cha VVU barani kote. Matokeo yake, mipango ya usimamizi wa madawa kwa ujumla (MDAs) kwa kutumia dawa praziquantel (PZQ) inaweza kuwa njia ya kuzuia FGS na maambukizi mapya ya VVU barani Afrika.