Nitajuaje ikiwa niko tayari kufanya ngono?
Watu huhisi wako tayari katika hatua tofauti. Ni juu yako kuamua wakati unaokufaa. Kuhisi wasiwasi kidogo ni kawaida - lakini pia ngono inapaswa kuwa ya kufurahisha, kitu ambacho unataka kufanya kwa dhati. Ikiwa unahisi kama unashinikizwa pengine ni ishara kwamba hauko tayari.
Hakuna sheria ambazo zinasema wakati ambapo unapaswa kufanya ngono kulingana na muda mliokuwa mkichumbiana. Ikiwa wewe unakuwa na furaha kuchumbiana lakini hutaki kufanya ngono, basi unapaswa tu kuendelea kufanya hivyo.
Ikiwa unafikiri kwamba uko tayari, zungumza na mwenzi wako kuhusu jinsi unavyohisi na kile ambacho ungependa kujaribu. Kabla ya kufanya ngono ni vizuri kuelewa machaguo yako ya uzuiaji mimba na jinsi ya kuzuia magonjwa ya zinaa.
Itakuwaje ikiwa mwenzi wangu ataonekana amesisimka na kuwa tayari kufanya ngono? Je, bado ninahitaji kupata ruhusa?
Wakati mwingine miili yetu itasisimuliwa lakini hatutaki kuguswa. Hata kama uume umesimama au uke una majimaji, si mwaliko wa kiotomatiki wa kufanya ngono. Akili zetu zinaweza kutaka kinyume cha kile miili yetu inafanya kitu ambacho kinaweza kusababisha kuchanganyikiwa na kuwa na wasiwasi. Ni lazima mara zote usikilize kile ambacho mtu anakuambia kwamba anakitaka, zaidi ya kile ambacho mwili wake unaonekana kukifanya. Kufikiri kwamba mwili wa mwezio umesisimuka si kisingizio kinachokubalika cha kuendelea kufanya ngono wakati mtu anakuomba uache.
Je, umri wa kuweza kutoa ruhusa unamaanisha nini? Na kwa nini upo?
Umri wa kuweza kutoa ruhusa’ ni njia nyingine ya kusema umri unaoruhusiwa kisheria kwamba unaweza kutoa ruhusa ya kufanya ngono. Nchi nyingi zina sheria zinazoelezea umri ambao mtu anapaswa kuwa nao kabla ya kukubali kufanya ngono. Umri wa kawaida wa ruhusa ya kufanya ngono ni miaka 16, lakini hii inaweza kutofautiana kutoka nchi hadi nchi.
Ikiwa mtu mzima atafanya ngono na mtu aliye chini ya umri wa kuweza kutoa ruhusa, anavunja sheria. Inajulikana kisheria kama ubakaji kwa sababu mtoto au kijana anachukuliwa kuwa ni mdogo kukubali kisheria. Hii inamaanisha kuwa hata ikiwa mtu aliye chini ya umri huu atasema 'ndio', kufanya ngono naye bado kunachukuliwa kuwa ubakaji.
Sheria hizi zipo ili kuwalinda watoto na vijana, ambao kwa sababu ya umri wao mdogo na utegemezi kwa watu wazima wako katika hatari zaidi ya kudhulumiwa na huenda wasiweze kuelewa kikamilifu ngono ili kutoa ruhusa sahihi.
Nifanyeje ikiwa mtu ananiambia kuhusu shambulio au unyanyasaji wa kingono?
Mambo mengi yanaweza kuwafanya watu waogope kuwaambia wengine kuhusu uzoefu wao wa shambulio au unyanyasaji wa kingono. Ikiwa mtu atachagua kukuambia kuhusu jambo lililompata, ni muhimu kwamba uheshimu imani yake na ujibu kwa njia ambayo ni nyeti na kuyatanguliza mahitaji yake. Si jambo rahisi la kupitia, lakini hapa kuna ushauri wa kukusaidia kumsaidia.
1. Jua kwamba kuzungumza kuhusu shambulio la kingono kunaweza kutia wasiwasi.
Sababu ya kawaida wanayotoa watu ya kutoripoti mashambulio ni kwamba waliogopa kuwa hawataaminika. Watu wanaweza pia kuwa na wasiwasi kwamba kwa namna fulani shambulio hilo litaonekana kama kosa la aliyeripoti. Fahamu hili na ujaribu kuepuka kusema maneno kama vile 'Siwezi kuamini'. Unaweza kuwa unamaanisha tu kusema kwamba umeshtuka, lakini anaweza kuichukulia kama umesema huamini kile anachokuambia. Ni muhimu kutambua kwamba unyanyasaji wa kingono unaweza kufanyika kwa mtu yeyote: wanaume, wanawake na watoto na kamwe si kosa la mwathiriwa. Ni vizuri pia kukumbuka kwamba kiwango cha shambulio hakibainishi ukali wake.
2. Jaribu kumzingatia pamoja na mahitaji yake.
Kusikia kuhusu unyanyasaji wa kingono kunaweza kushtua na kukasirisha, lakini ni muhimu kumhakikishia na kumsikiliza mtu huyo. Jaribu kutoonekana kushtuka na kuogopa, kwani mtu huyo anaweza kuwa na wasiwasi juu ya kukukasirisha. Unapaswa pia kuepuka kuuliza maswali mengi sana kuhusu maelezo. Hii inaweza kufanya mambo kuwa magumu ikiwa ataamua kuwaambia polisi na anaweza kuwa hayuko tayari au anataka kukuambia maelezo yote kuhusu kile kilichotokea. Kuzungumza kuhusu unyanyasaji wa kingono kunaweza kuwa vigumu. Mwache aamue jinsi na wakati anaotaka kulizungumzia.
3. Heshimu usiri yake.
Taarifa hii inapaswa kuchukuliwa kwa uangalifu. Ikiwa unahitaji kuripoti tukio hilo kwa mtu mwingine au la itategemea hali hiyo na uhusiano wako na mtu huyo. Kwa upande wa watoto au unapokuwa na jukumu la kumtunza mtu huyo utahitaji kuripoti tukio hilo, lakini vinginevyo kile alichokuambia kinapaswa kuchukuliwa kama maelezo ya siri na kisitolewe kwa mtu mwingine yeyote isipokuwa uwe na ruhusa yake. Mtu wa kumwambia ni chaguo lake. Ikiwa huna uhakika ikiwa unahitajika kuripoti taarifa hii, zungumza na msimamizi au mwajiri kuhusu ni lipi litakuwa jukumu lako katika hali hizi.