Kuna uhusiano gani kati ya kiwango cha virusi kwenye damu na CD4?
Kiwango cha CD4 na vipimo vya kiwango cha virusi kwenye damu hupima vitu tofauti. Kipimo chako cha kiwango cha virusi kwenye damu hupima kiwango cha VVU katika mwili wako ilhali kiwango cha CD4 hupima afya ya mfumo wako wa kinga kwa kuhesabu ni seli ngapi za CD4 ulizonazo. Kiwango chako cha virusi kwenye damu ni bora kwa kupima jinsi matibabu yako yanavyofanya kazi vizuri, ilhali kiwango chako cha CD4 husaidia wahudumu wa afya kuelewa ikiwa una uwezekano wa kuendelea kuwa na afya nzuri.
Ingawa ni tofauti, kiwango chako cha CD4 na kiwango cha virusi kwenye damu mara nyingi huunganishwa. Kadiri kiwango chako cha virusi kwenye damu kinavyoongezeka, VVU huharibu zaidi seli zako za CD4 na kusababisha kiwango chako cha CD4 kupungua. Unapoanza matibabu kiwango chako cha virusi kwenye damu kitapungua, hali inayoruhusu kiwango chako cha CD4 kupanda, huku mfumo wako wa kinga ukijirekebisha na kujijenga upya.
Kwa ujumla, kiwango chako cha CD4 hupokea polepole zaidi mabadiliko katika mwili wako. Kiwango chako cha virusi kwenye damu kitapanda na kushuka haraka zaidi ili kukabiliana na matibabu kufanya kazi au kushindwa,huku kiwango cha CD4 kikichukua muda zaidi kubadilika. Hii ndiyo sababu inayofanya vipimo vya kiwango cha virusi kwenye damu kuwa njia inayopendelewa ya kufuatilia matibabu yako.
Ninaweza kufanya nini ili kusimamia vizuri hali yangu mwenyewe?
Ni muhimu kujenga uhusiano wa uaminifu na timu yako ya huduma ya afya, kwani utaonana nao kwa muda mrefu. Kadiri unavyowasiliana nao na kuwaambia jinsi unavyoendelea, ndivyo utakavyopata huduma bora.
Ili kufaidika zaidi kutokana na miadi yako, kuandaa na kuandika maswali yoyote uliyo nayo kabla ya miadi kutakusaidia. Hii itakusaidia kukumbuka ikiwa kuna mambo uliyotaka kuwaambia. Ni sawa kukatiza na kuuliza maswali ikiwa huelewi kile ambacho mhudumu wako wa afya anakuambia. Unapaswa kuelewa dawa yoyote unayotumia, vipimo unavyofanya au uchunguzi wowote na rufaa uliyonayo. Jinsi unavyoelewa zaidi, ndivyo ilivyo bora kwa sababu inakusaidia kuisimamia afya yako na itakufanya uhisi kuwa na udhibiti zaidi.
Ikiwa unakutana na timu nyingi za wahudumu wa afya kwa shida tofauti za kiafya, ni lazima timu hizo ziwasiliane na kujua ni huduma gani nyingine za afya au matibabu ambayo unatumia. Hii itawasaidia kuhakikisha kuwa hakuna mwingiliano mbaya.
Ikiwa una matatizo, fahamu mahali unapoweza kwenda kuwasilisha malamiko. Inaweza kuwa mhudumu wa afya wa ngazi ya juu zaidi wa afya au mtu mwingine katika jamii yako au mfumo wa huduma ya afya.
Dhibiti miadi yako vizuri. Unapaswa kujaribu kuhakikisha unajua ni lini utarudi tena kabla ya kuondoka na uweke nafasi tena ya miadi yoyote ambayo huwezi kuifanya.
Nitapata ukaguzi gani mwingine wa afya?
Ukaguzi wa afya unaopata utategemea matibabu unayotumia. Unaweza pia kuwa na ukaguzi tofauti wa kiafya kulingana na kiwango chako cha CD4. Kwa ujumla wahudumu wako wa afya watakuwa na haja ya kufuatilia:
a) viwango vya sukari katika damu yako - hivi vinaonyesha jinsi mwili wako unavyopata nguvu kutoka kwenye chakula
b) afya ya ini lako - kuhakikisha kuwa unaweza kuchakata vyema matibabu yako ya kupunguza makali ya virusi vizuri
c) Utendaji wa figo yako - kuangalia ikiwa zinaweza kuondoa taka vizuri kutoka kwenye mwili wako
d) kiasi cha mafuta katika damu yako, uzito wa mfupa wako na afya ya ngono.
Unapaswa pia kupimwa maambukizi mengine ya magonjwa ya zinaa, hepatitisi B na C pamoja na kifua kikuu.Vipimo hivi
vingi vitafanywa kwa kupima damu au sampuli ya mkojo. Daktari wako anapaswa kuelezea vipimo anavyofanya na unapaswa kuripoti maswala mengine yoyote au mabadiliko ambayo unagundua katika afya yako. Hii itawasaidia kukupa huduma inayofaa.