Nifanye nini ikiwa kondomu imepasuka?
Kondomu ni za kuaminika sana maadamu unazitumia kwa usahihi. Hata hivyo, ikiwa kondomu imepasuka, usishtuke - fuata hatua hizi rahisi:
1. Ondoa uume haraka
2. Usioshe kwenye njia ya haja kubwa au ukeni kwani hii inaweza kueneza maambukizi
3. Ikiwa unahitaji kufanya hivyo, nenda kwenye kituo cha huduma ya afya ili kupata kingamimba ya dharura au Dawa zinazotumika baada ya kuwa katika hatari ya VVU (PEP)
4. Pata kipimo cha VVU na Magonjwa ya zinaa
Ili kuzuia kondomu kupasuka, hakikisha unaivaa kwa usahihi, tumia kilainishi kinachotokana na maji na tumia kondomu moja tu kwa wakati mmoja.
Kondomu zina ufanisi kwa kiasi gani?
Zikitumika kwa usahihi ni vigumu sana kondomu kutofanya kazi vyema. Kabla ya kuuzwa, kondomu hupitia kipimo cha uhakikisho wa ubora. Hii inamaanisha kwamba watu wanaozitengeneza wanafanya ukaguzi ili kuhakikisha kwamba zinakidhi viwango vya juu vinavyohitajika ili kukupa ulinzi. Ili mradi haijapita tarehe ya muda wa matumizi, kondomu haipaswi kuwa na tatizo lolote. Hata hivyo, ni bora kununua kondomu kutoka kwa chapa au wauzaji unaowaamini.
Ili kondomu ziwe na ufanisi, lazima:
1. uitumie kila wakati unapofanya ngono
2. uivae kabla ya kuanza kufanya ngono
3. uivae wakati wote unapofanya ngono
4. ufuate maelekezo ya jinsi ya kutumia kondomu kwa usahihi.
Kondomu zinafaa kwa kila aina ya ngono na unaweza kuongezea ufanisi wake kwa kutumia kilainishi.
Ikiwa tuko katika uhusiano je, tunaweza kuacha kutumia kondomu?
Uamuzi wa kutumia au kutotumia kondomu ni wa kufanya pamoja kama wenza. Inaweza kutegemea mambo kadhaa, kwa mfano, ikiwa una Kiwango cha VVU kwenye damu yako kisichogundulika, ikiwa mwenzi wako anataka kutumia Vidonge vya kumeza mara kwa mara vya kuzuia VVU (PrEP), ikiwa mmoja wenu anafanya ngono na mtu mwingine yeyote na ikiwa mnapanga familia. Kuna mambo mengi zaidi yanayoweza kuathiri uamuzi wenu. Ni muhimu kwamba hakuna mwenzi anayehisi kushinikizwa kufanya kitu ambacho hajaridhishwa nacho. Si lazima uache kutumia kondomu ili kuthibitisha kuwa unampenda au unamwamini mwenzi wako, kuna njia zingine nyingi za kuonyesha kuwa unajali.
Kabla ya kuacha kutumia kondomu, unapaswa kuwa na uhakika kwamba una Kiwango cha VVU kwenye damu yako kisichogundulika au kwamba mwenzi wako anatumia Vidonge vya kumeza mara kwa mara vya kuzuia VVU (PrEP) (au njia zote mbili). Unapaswa pia kufanya vipimo vya magonjwa ya zinaa na ikiwa hamko tayari kupata mtoto unaweza kutumia machaguo mengine ya kingamimba. Kumbuka kwamba kondomu ndio njia pekee ya kingamimba ambayo pia inakulinda dhidi ya VVU na magonjwa mengine ya zinaa.