Boost

Kuna kiasi kidogo cha VVU kwenye mate ya mtu mwenye VVU ambapo maambukizi hayawezi kusambazwa kwa kubusiana. Lakini hali hii huwachanganya watu wengi kwamba unaweza kutumia sampuli za mdomo kupima VVU.

Ili kufafanua suala hili, jambo la kwanza la kufahamu ni kwamba vipimo vya mdomo vya VVU havitambui virusi vyenyewe, badala yake hutafuta ‘kingamwili’. Hizi ni seli ambazo mfumo wa kinga hupata ili kukabiliana na maambukizi ya VVU. Kwa hivyo, majimaji ya mdomoni hayana virusi vinavyohitajika ili kupitisha maambukizi ya VVU, lakini yana kingamwili zinazohitajika ili kutambua maambukizi ya VVU.

Inafaa pia kuzingatia kwamba vipimo havitafuti kingamwili kwenye mate, badala yake hupima kitu kiitwacho ‘majimaji ya utando telezi wa mdomoni’, ambayo ni majimaji yanayotolewa kutoka kwenye seli zinazounda mashavu na fizi zako. Hii ndiyo sababu unapochukua sampuli ya mdomoni unasugua kipimo kwenye fizi na mashavu yako, ambapo kuna uwezekano mkubwa wa kingamwili kupatikana.

Ingawa hivi sasa inapendekezwa kwamba huduma ya kujifanyia vipimo iwe mojawapo ya chaguo katika nchi mbalimbali, bado zana za kujifanyia vipimo hazipatikani kila mahali.

Ikiwa vipimo vinapatikana au havipatikani katika eneo ulipo, itategemea pia ikiwa kliniki iliyo karibuni nawe ina vifaa hivyo.

Ili kujua kama kuna vifaa vya kujipima vinavyopatikana karibu nawe muulize mhudumu wa afya.

ilimradi mtu anayepima amevuka kipindi cha kugundulika kwa VVU, kujifanyia vipimo hutoa majibu sahihi kama vipimo vya maabara kwa kubaini majibu ya kutokuwa na maambukizi. Kujifanyia vipimo kwa njia ya mdomo ni sahihi kwa asilimia 99.9 kwa majibu ya kutokuwa na maambukizi. Hii humaanisha kwamba ilimradi tu kipindi cha kugundulikwa kwa VVU kimepita na vipimo vimetumika kwa usahihi, vipimo kwa njia ya mdomo vina uwezekano mdogo sana wa kutoa majibu ya uongo ya kutokuwa na maambukizi (kumwambia mtu kwamba hana VVU, wakati kwa kweli, anavyo).

Vipimo vya kujifanyia vina uwezekano mkubwa wa kutoa majibu ya uongo ya kuwa na maambukizi kuliko vipimo vya kawaida vya maabara. Hii ndiyo sababu inashauriwa kuwa majibu yote ya kuwa na maambukizi yathibitishwe katika kliniki. Baada ya kuthibitishwa, unaweza kufahamu kuwa majibu ni sahihi na kupata huduma unayohitaji.