Kwa nini kipimo cha mapema kwa mtoto mchanga ni kipaumbele?
Kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto imekuwa moja ya mafanikio makubwa ya kukabiliana na VVU. Hivi sasa tunaona akina mama wengi wanatumia matibabu ya kupunguza makali ya VVU (ART) na maambukizi ya VVU kwa watoto yanapungua.
Hata hivyo, maendeleo katika upimaji wa mapema wa watoto wachanga yamekuwa ya polepole zaidi. Mnamo mwaka wa 2019, chini ya asilimia 60 ya watoto walipimwa VVU katika wiki 8 za kwanza, na ni asilimia 53 tu ya watoto wenye VVU walikuwa wameanza matibabu ya kupunguza makali ya VVU (ART) katika maeneo mengi. Hii sasa ni mojawapo ya vipaumbele vikubwa kwa wahudumu wa VVU. Bila kupimwa na kupata matibabu, watoto wachanga wanakabiliwa na hatari kubwa ya kifo au ugonjwa mbaya. Kuboresha upimaji kutahakikisha kwamba watoto wengi zaidi walio na VVU wanaweza kuendelea kuishi maisha marefu na yenye afya.
Utambuzi unavyofanywa kwa mashine za kupima damu hurejela nini na husaidia vipi?
Katika maeneo mengi, kunaweza kuwa na ucheleweshaji wa muda mrefu kati ya mtoto anapopimwa na wakati wa kupokea majibu yake. Hii ni kwa sababu sampuli lazima zipelekwe kwenye maabara (ambazo mara nyingi ziko mbali) ili kupata majibu.
Kipindi hiki kirefu cha kusubiri majibu huchelewesha watoto wachanga kuanza matibabu na katika baadhi ya matukio inaweza kumaanisha kuwa majibu hayachukuliwi kabisa na watoto wanaachwa bila kutambuliwa hali zao.
Shirika la Afya Ulimwenguni linapendekeza kwamba majibu ya vipimo vya watoto wachanga yarudishwe kwa familia kabla ya siku 30 baada ya mtoto kupimwa. Hata hivyo, wastani wa muda wa kusubiri unaweza kuwa hadi siku 55, kumaanisha kwamba watoto mara nyingi hawaanzishiwi matibabu ya kupunguza makali ya VVU kwa miezi muhimu ya mwanzo wakati hatari yao ya kifo ni kubwa zaidi.
Vifaa vipya vya Vipimo vinavyofanywa kwa mashine za kupima damu vinamaanisha kuwa sampuli za vipimo vya watoto wachanga si lazima zipelekwe kwenye maabara kwa ajili ya kuchakatwa. Badala yake, wahudumu wa afya katika kliniki wanaweza kushughulikia vipimo wenyewe na kuzipa familia majibu. Hii ina maana kwamba majibu yanaweza kurejeshwa kwa familia siku hiyo hiyo na watoto wanaweza kuanza matibabu haraka. Hii inaepusha majibu kutochukuliwa na hali za kiafya za watoto kuachwa bila kutambuliwa.
Vipimo hivi tayari vinatumika katika baadhi ya kliniki nchini Zimbabwe, Kenya, Malawi, Tanzania, Afrika Kusini na Msumbiji, ambako vimepata matokeo mazuri. Katika kisa kimoja, idadi ya watoto wanaoanza matibabu ya kupunguza makali ya VVU ndani ya siku 60 iliongezeka kutoka asilimia 43.3 na upimaji wa kimaabara hadi asilimia 92.3 baada ya Vipimo vinavyofanywa kwa mashine za kupima damu kuanzishwa.
Vipimo vya papo hapo mara nyingi hufanya kazi kwa gharama nafuu, na baadhi ya vifaa vinaweza pia kutoa kipimo cha kiwango cha VVU kwenye damu pamoja na kifua kikuu.