Kwa nini usugu wa dawa (dawa kutofanya kazi) ni tatizo zaidi kwa watoto?
Kuna sababu kadhaa za watoto kuwa katika hatari kubwa ya kupata usugu wa dawa za VVU (dawa za VVU kutofanya kazi). Baadhi ya sababu hizo zinahusiana na wao kutegemea watu wazima wanaowazunguka, zingine zinahusiana na chaguo za matibabu yao.
Kwa sababu watoto wanategemea walezi wao kuwasaidia kufuata ratiba ya matibabu, wako katika hatari zaidi ya kushindwa kupata matibabu. Walezi wengi watakuwa na VVU wao wenyewe na wanaweza kuwa na changamoto zao za kufuata utaratibu wa matibabu. Hii inaweza kufanya usimamizi wa dawa za mtoto kuwa mgumu zaidi, haswa ikiwa mtoto wake atalazimika kupata matibabu yake kwa nyakati tofauti za siku na mara tofauti. Pale ambapo utunzaji wa watoto ni tofauti na utunzaji wa watu wazima wenye VVU, wazazi na walezi wanaweza kulazimika kuhudhuria miadi mingi, ikimaanisha kusafiri zaidi kwenda na kutoka kwenye kliniki jambo linalowanfanya kuchoka zaidi.
Kuhakikisha kuwa watoto wanapata matibabu sahihi ya kupunguza VVU pia inaweza kuwa ngumu zaidi. Kwa mfano kupata dozi yao sahihi ni ngumu zaidi kwani unahitaji kuhakikisha kuwa dawa ina nguvu ya kutosha kudhibiti virusi, lakini isiwe kali sana na kuwa na athari mbaya. Kadiri watoto wanavyokua, dozi wanayohitaji itabadilika na kuongezeka ili kulingana na uzito wao mpya wa mwili. Ikiwa dozi yao ni ya chini sana wako katika hatari ya kupata usugu wa dawa.
Kwa sababu watoto huanza matibabu wakiwa na umri mdogo, watakuwa wakitumia dawa kwa muda zaidi. Kadiri unavyofanya matibabu kwa muda mrefu ndivyo unavyoweza kupata usugu wa dawa. Lakini uzingatiaji mzuri wa matibabu unaweza kudhibiti hatari hii.
Kwa nini kuna machaguo machache ya matibabu ya kupunguza makali ya VVU kwa watoto?
Kwa bahati mbaya kuna machaguo machache ya matibabu yanayopatikana kwa watoto. Mojawapo ya sababu za hii ni kwamba matibabu mengi mapya hupimwa kwa watu wazima kwanza. Ni baada tu ya dawa kuonekana kufanya kazi kwa watu wazima ndipo watafiti wataanza kufikiria kutengeneza matoleo ya matibabu kwa ajili ya watoto. Hii inamaanisha kuwa matibabu mengi ya watoto yana miaka michache nyuma ya yale yanayopatikana kwa watu wazima. Watoto pia wanaweza kuhitaji dawa zirekebishwe ili ziweze kuwa na ladha nzuri na kuja katika vidonge vidogo.
Mojawapo ya sababu zinazowafanya watu wazima kutumiwa kupima dawa kwanza ni kwamba ni rahisi kuelewa madhara ya matibabu katika mwili wa mtu mzima. Miili ya watoto inabadilika na kukua kila wakati, kwa hivyo ni ngumu zaidi kuelewa athari za matibabu. Pia kuna miongozo na sheria za kimaadili zaidi kuhusu jinsi ya kuwashirikisha watoto katika kujaribu dawa, kwani hii inaweza kuwaweka katika hatari fulani.
Mafanikio yetu katika kuweza kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito, kuzaliwa na kunyonyesha, yalimaanisha kuwa idadi ya watoto wanaozaliwa na VVU inapungua. Hii ni habari njema kwa afya ya watoto, lakini inamaanisha kuwa soko la dawa za watoto za kupunguza makali ya virusi pia linazidi kupungua. Matokeo yake ni kwamba, kampuni zinasimamisha kutengeneza dawa kwa ajili ya watoto wenye VVU. Kuanzisha matibabu mapya ni ghali na kampuni za dawa zinataka kujua kwamba zitaweza kuuza dawa mara tu zitakapokuwa tayari, ili kurejesha baadhi ya gharama zao. Hii si hakika ikiwa kutakuwa na watoto wachache wanaohitaji matibabu katika siku zijazo.