Je, mbona kutoweza kugundulika humaanisha kuwa huwezi kusambaza VVU kwa watu wengine? Tunajua hili kwa kweli?
Kupokea Matibabu ya kupunguza makali ya VVU ukiwa na VVU hupunguza kiasi cha VVU mwilini mwako. Kadiri unavyokuwa na virusi vichache mwilini mwako, ndivyo utakavyokuwa na virusi vichache katika shahawa yako, majimaji ya ukeni au unyevu wa kwenye sehemu ya haja kubwa. Hii inamaanisha kuwa una uwezekano mdogo wa kuambukiza VVU wakati wa ngono. Ukizingatia matibabu yako na yanaendelea vizuri, inaweza kufika mahali ambapo kiwango cha virusi mwilini mwako ni kidogo sana kiasi kwamba vipimo vya kawaida vitashindwa kugundua. Hiki ndicho kinachoitwa ‘kiwango cha virusi kwenye damu kisichoweza kugundulika’. Mara nyingi imeainishwa kuwa wakati ambapo kiasi cha VVU katika damu yako kiko chini ya nakala 50/ml – kulingana na kipimo cha kiwango cha VVU kwenye damu. Ikiwa una kiwango cha VVU kwenye damu kisichoweza kugundulika, unakuwa umeondoa VVU kwa kiwango ambacho huwezi tena kuieneza kupitia ngono.
Hii ilithibitishwa mnamo mwaka 2016, katika utafiti ambao ulijumuisha wenzi 548 wa jinsia tofauti. Katika wanandoa wote mwenzi aliyekuwa na VVU alikuwa na kiwango cha virusi ambacho hakigunduliki. Hakuna maambukizi ya VVU yaliyotokea kwa wanandoa hawa licha ya kuwa na matukio mengi ya ngono bila kinga. Ili kujua ikiwa una kiwango cha virusi kisichogundulika lazima uwe na mpango wa ufuatiliaji wa kiwango cha VVU kwenye damu yako. Ikiwa unafuata vizuri matibabu yako na hauna shida yoyote basi kuna sababu nzuri ya kufikiria kuwa kiwango cha VVU kwenye damu yako kitakuwa chini. Lakini huwezi kuwa na uhakika kwamba una kiwango cha virusi kisichogundulika isipokuwa uwe umepima kiwango cha VVU kwenye dau yako. Kwa bahati mbaya, hii inamaanisha kwamba watu wasio na uwezo wa kufikia ufuatiliaji wa kiwango cha VVU katika damu hawatajua kwa uhakika ikiwa wana kiwango cha virusi kisichogundulika.
Je, unaweza kupata VVU kutokana na vifaa vya kufanya ngono au kupiga punyeto?
Ili kupata VVU viowevu vya ngono kutoka kwa mtu mmoja lazima viingie kwa mtu mwingine. Hii haitokei kwa kwa kupiga punyeto. Ikiwa unashiriki kifaa cha kufanya ngono kinachoingizwa, hatari ni ndogo, lakini bado inashauriwa kwamba uoshe kifaa hicho kabla ya kutumia na utumie kondomu mpya kwa kila mtu. Ingawa uwezekano ni mdogo sana wa kupata VVU kwa kushiriki vifaa vya ngono, ni rahisi kusambaza maambukizi mengine ya zinaa (magonjwa ya zinaa) kama vile klamidia na kisonono kwa njia hii. Kufuata ushauri huu utakulinda dhidi ya haya.
Je, VVU bado vitasambazwa kwa wengine iwapo nitafanya ngono wakati wa hedhi?
Ndiyo, damu ya hedhi na majimaji mengine ya ngono yanaweza kuwa na VVU. Ikiwa una VVU, kiwango chako cha VVU kwenye damu kinaweza kuwa juu zaidi ukiwa kwenye hedhi. Hii inamaanisha kuwa una uwezekano mkubwa wa kuambukiza VVU wakati huu. Ikiwa huna VVU, bado unaweza kupata VVU ikiwa unafanya ngono wakati wa hedhi. Unapokuwa kwenye hedhi, mabadiliko katika uke wako hufanya iwe rahisi kwa VVU kuingia mwilini mwako.
Kutumia kondomu, kuwa kwenye matibabu yenye ufanisi na kutumia Vidonge vya kumeza mara kwa mara vya kuzuia VVU (prEP) yote hupunguza hatari hizi.