Je, wataniuliza maswali ya aina gani, ikiwa ninataka kutumia PEP?
Kabla ya kukuandikia PEP, mhudumu wa afya atahitaji kuelewa hatari zilizokukumba. Atahitaji kuhakikisha kuwa kuna hatari ya kweli ya kuambukizwa VVU. Kuna njia fulani tu ambapo VVU vinaweza kuambukizwa, kwa hivyo iwapo hizi hazihusiki nawe, huhitaji kutumia PEP.
Atakuuliza mambo uliyofanya. Iwapo ulifanya ngono isiyo salama, anaweza kuhitaji kujua aina gani (ya ukeni, katika njia ya haja kubwa au ya mdomoni) na iwapo unajua hali ya VVU ya mwenzio. Maswali yake hayakusudii kukukera na hutakiwa kuhisi kuwa mtu huyo anakusema vibaya, anajaribu tu kukutafutia huduma bora ya matibabu.
Je, nitahitaji kutumia kondomu ninapotumia PEP?
Ndiyo, inashauriwa uendelee kutumia kondomu unapotumia PEP. Hii ni kwa sababu huenda dawa hizo za PEP zisifanye kazi vizuri iwapo utakuwa katika hatari ya VVU tena upoendelea kutumia Dawa hizo. Kwa bahati mbaya, PEP hazina ufanisi kwa asilimia 100. Hata kama unatumia PEP, bado kuna uwezekano kuwa hazitafanya kazi. Kutumia kondomu unapotumia PEP humaanisha kuwa unazuia kuwaambukiza VVU wenza wako. Pia, PEP hazizuii mimba au magonjwa mengine ya ngono, kwa hivyo ni vyema kuendelea kutumia kondomu.
Je ni mara ngapi mtu anaweza kupata Dawa PEP?
Ingawa hakuna kikomo cha mara unazoweza kutumia PEP, hazikusudiwi kutumiwa siku zote, au kama kinga ya mara kwa mara. Ukiona kuwa unahitaji kutumia PEP, unashauriwa uzungumze na mhudumu wa afya kuhusu njia nyingine za kuzuia kupata VVU. Dawa zinazotumika kabla ya kuwa katika hatari ya VVU (PrEP) zinaweza kukupa kinga ya kudumu dhidi ya VVU na ni njia ya kuaminika ya kuzuia maambukizi kuliko PEP.