Kifua kikuu sugu kwa dawa nyingi ni nini?
Kifua kikuu kinaweza kuwa sugu kwa dawa mbili zenye nguvu zaidi ambazo tunapaswa kutumia kukitibu - isoniazid na rifampicin. Ikiwa maambukizi ya Kifua kikuu hayawezi tena kutibiwa na mojawapo ya dawa hizi, inabainishwa kama Kifua kikuu sugu kwa dawa nyingi.
Kifua kikuu sugu kwa dawa nyingi ni tatizo kubwa. Kwa kawaida matibabu ya Kifua kikuu huwa na ufanisi wa asilimia 90, lakini kwa mwili kukataa dawa, ufanisi huu hupungua hadi asilimia 50. Kifua kikuu sugu sana kinaweza kutokea ikiwa Kifua kikuu cha mtu ni sugu kwa matibabu mengine ya mstari wa pili pamoja na isoniazid na rifampicin. Ni theluthi moja tu ya watu walio na Kifua kikuu sugu kwa dawa wataponywa.
Kifua kikuu sugu kwa dawa nyingi kina uwezekano mkubwa wa kupatikana wakati mtu hafuati matibabu. Hii wakati mwingine inaweza kuwa matokeo ya kliniki kutoshughulikia utunzaji wao vizuri, kwa mfano, ikiwa hawampi mgonjwa dawa anazohitaji kwa wakati unaofaa. Inaweza pia kutokea ikiwa mtu anapata shida kupata matibabu.
Ambapo Kifua kikuu chenye usugu kwa dawa ni cha kawaida katika jamii, inawezekana kuambukizwa aina ya Kifua kikuu ambayo tayari ina usugu kabla ya kuanza matibabu.
Watunga sera na wataalamu wa huduma za afya kote ulimwenguni wanatafuta njia za kukabiliana na kuongezeka kwa Kifua sugu kinachokataa dawa nyingi. Kwa sasa, jambo muhimu zaidi ni kwamba watu wapate matibabu yao vizuri na wapate msaada unaofaa kuhusu uzingatiaji.
Je, kuna chanjo ya Kifua kikuu?
Ndiyo, chanjo ya BCG inaweza kukinga dhidi ya Kifua kikuu. Chanjo hii ni bora sana dhidi ya aina kali zaidi za Kifua kikuu, ikitoa kinga hadi asilimia 80, hata hivyo, kinga dhidi ya Kifua kikuu cha mapafu iko chini kidogo.
Miongozo ya nani anapaswa kupewa chanjo itatofautiana kulingana na mahali ulipo ulimwenguni. Kwa nchi zilizo na viwango vya juu vya Kifua kikuu, Shirika la Afya Ulimwenguni linapendekeza kuwapa watoto wachanga chanjo ya BCG wanapozaliwa. Hata hivyo, halipendekezi kwa watoto ambao wanaweza kuwa na VVU, kwa sababu watoto walio na VVU wanaweza kupata ugonjwa kama wa Kifua kikuu kutokana na chanjo
Je, kwa nini ni muhimu kuzingatia matibabu yangu ya Kifua kikuu?
Bakteria ya Kifua kikuu hufa polepole. Ili kuhakikisha kuwa bakteria wote wameondoka unapaswa kuendelea kutumia dawa yako kama ilivyoagizwa kwa muda wote. Unaweza kuanza kujisikia vizuri haraka, lakini ni lazima uendelee kupata matibabu yako hadi mwisho kama ulivyoagizwa.
Usipomaliza dawa zako zote au ukitumia kwa njia isiyo ya kawaida, inaweza kuacha kufanya kazi. Hii ni kwa sababu ikiwa haujapata dawa ya kutosha mwilini mwako, bakteria bado wataweza kukua na watajifunza jinsi ya kushinda dawa. Hii inamaanisha kuwa katika siku zijazo ugonjwa wako wa Kifua kikuu utakuwa ni ngumu kutibiwa. Ikiwa ugonjwa wako wa Kifua kikuu unakuwa sugu nafasi ya kupona itakuwa ndogo na unapaswa upate matibabu kwa muda mrefu.s
DOT ni nini?
Njia moja ya kuwasaidia watu kupata matibabu yao mara kwa mara ni 'tiba ya uangalizi wa karibu' (DOT). DOT ni njia ya kupata matibabu. Inajumuisha kukutana na mhudumu wa afya katika kliniki, katika jamii au nyumbani, ili watazame na kuhakikisha kuwa unatumia dawa yako kwa usahihi. Ni njia inayotumika sana kwa matibabu ya kifua kikuu na inaweza kusaidia hasa katika hali ambapo mtu ana ugumu wa kuzingatia matibabu.
DOT hufanya kazi vizuri wahudumu wa afya wanapotumia mikutano hii kuwapa wagonjwa msaada wa ziada. Hii inaweza kujumuisha kuwasaidia kutazama madhara au kutoa ushauri. Shirika la Afya Ulimwenguni kwa sasa linachunguza ikiwa simu za video zinaweza kutumika kama njia ya kutoa huduma ya DOT kwa njia ya gharama na muda unaofaa zaidi.