Je, hatua za ujauzito ni zipi?
Ujauzito huanza wakati manii hurutubisha yai. Kuanzia hapo mimba hugawanywa katika hatua tatu zinazoitwa trimesta. Kila moja huelezea hatua ya ukuaji wa mtoto wakati wa ujauzito.
Katika trimesta ya kwanza, yai huwa limerutubishwa na mwili wako unajiandaa kwa ujauzito. Unaweza kuhisi kuvutika kwa tumbo lako, kujihisi mgonjwa na kuhitaji kukojoa mara kwa mara wakati uterasi yako inavutika na kuanza kufinya kibofu chako cha mkojo.
Ni wakati huu ambapo mtoto wako anakua kutoka mkusanyiko wa seli hadi kuwa kiinitete. Viungo vyake na sehemu za mwili huanza kuundwa pamoja na kondo la uzazi. Kondo la uzazi ni kiungo ambacho kimeambatanishwa na ukuta wa tumbo lako la uzazi wakati wa ujauzito. Ni kupitia kondo la uzazi ambapo oksijeni, virutubisho na homoni zote hupitishwa kutoka kwako kwenda kwa mtoto wako.
Katika trimesta ya pili, ujauzito wako huonekana zaidi - ingawa muda halisi wa hatua hii utatofautiana kutoka kwa mwanamke hadi mwingine. Kawaida ugonjwa ambao mara nyingi hutokea katika trimesta ya kwanza utaanza kupungua. Unaweza pia kuhisi mtoto wako anaanza kusonga tumboni kuanzia karibu wiki 18 hadi 20.
Katika trimesta ya pili viungo vya mtoto wako huendelea kukua. Masikio yake kwa kawaida hukua kwa takribani wiki 16 ambayo inamaanisha kuwa ataanza kusikia sauti fulani. Kwa wakati huu mtoto atalala na kuamka, na anaweza kupiga mateke na kujinyoosha pia.
Trimesta ya tatu ni hatua ya mwisho ya ujauzito. Unaweza kuhisi uchovu na kukosa pumzi tumbo lako linaposukumwa kuelekea kwenye mapafu yako.
Kufikia hatua hii, sehemu kubwa ya ukuaji wa mtoto huwa imekamilika. Mifupa ya mtoto itaanza kuwa migumu na itaanza kupata mafuta. Mtoto pia kwa kawaida atageuka ili kichwa chake kielekezwe chini tayari kwa kuzaliwa.
Kwa nini folic acid ni muhimu katika ujauzito?
Folic acid ni kirutubisho muhimu sana kwa kina mama wote wajawazito. Husaidia ukuaji wa mtoto wako na humlinda dhidi ya kupata kasoro za kuzaliwa zinazojulikana kama kasoro za mrija wa neva, ambazo zinaweza kuathiri ubongo wa watoto, uti wa mgongo na mifumo ya neva.
Unapaswa kuanza kuitumia unapojaribu kupata ujauzito au mara tu utakapogundua kuwa una ujauzito.
Virutubisho vya folic acid hutumiwa kama kidonge. Unaweza pia kuongeza ulaji wako wa folic acid kwa kuhakikisha unakula mboga nyingi za majani, mchele wa kahawia na mkate wa kahawia. Ingawa kula zaidi vyakula vya aina hii ni vizuri, haitakupa folic acid yote ambayo mtoto wako anahitaji, kwa hivyo hakikisha kwamba unatumia virutubisho pia.
Ninawezaje kumkinga mtoto wangu dhidi ya kaswende pia?
Kaswende ni maambukizi mengine ambayo yanaweza kuambukizwa kwa urahisi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito. Inaweza kuwa hatari sana kwa watoto wachanga na mara nyingi husababisha kifo. Asilimia 40 ya watoto wanaozaliwa na kina mama walio na kaswende ambayo haijatambuliwa hufa kutokana na maambukizi.
Hii ndiyo sababu ni muhimu sana kupima kaswende wakati wa ujauzito. Unapaswa kupimwa kaswende katika miadi yako ya kwanza baada ya kugundua kuwa una ujauzito. Ikiwa una maambukizi hayo, kaswende inaweza kutibiwa na kiua vijasumu. Hii pia inaweza kuzuia maambukizi kusambazwa kwa mtoto wako. Ikiwa huna maambukizi ni muhimu uepuke kupata kaswende wakati wa kipindi chote cha ujauzito na unapaswa kupima tena ikiwa unafikiri unaweza kuwa katika hatari.
Si watoto wote wanaozaliwa na kaswende wataonyesha dalili za maambukizi, kwa hivyo ikiwa ulikuwa na kaswende wakati wa ujauzito wako na haukupata matibabu, mtoto wako atahitaji kupimwa wakati wa kuzaliwa. Ikiwa ana maambukizi, ni muhimu apate matibabu mara moja.