Tohara ya Hiari ya Kimatibabu kwa Mwanaume (VMMC) ina ufanisi kwa kiasi gani?
Tohara ya Hiari ya Kimatibabu kwa Mwanaume (VMMC) haifanyi isiwezekane kwa mtu kupata VVU, bali hufanya uwezekano uwe mdogo. Utafiti umeonyesha kuwa tohara kwa mwanaume inaweza kupunguza maambukizi kutoka kwa mwanamke kwenda kwa mwanaume kwa asilimia 60.
Tohara ya Hiari ya Kimatibabu kwa Mwanaume ni uingiliaji kati wa mara moja utakaokuwa na athari ya muda mrefu katika kupunguza hatari ya wewe kupata VVU. Njia hii ni njia rahisi na yenye ufanisi ya kuongeza kinga yako dhidi ya virusi. Hata hivyo, wanaume ambao wametahiriwa wanapaswa kutumia njia zingine za kuzuia VVU ikiwa ni pamoja na kutumia kondomu, kupunguza idadi ya wenzi wa kingono na kufanya vipimo vya mara kwa mara vya VVU na magonjwa ya zinaa.
Je, Tohara ya Hiari ya Kimatibabu kwa Mwanaume (VMMC) inapendekezwa kwa wanaume wanaoshiriki ngono na wanaume?
Tohara ya Hiari ya Kimatibabu kwa Mwanaume hupunguza hatari ya kupata VVU kwa kufanya ngozi iliyo juu ya uume kuwa ngumu. Kwa sababu hii, inaweza tu kupunguza hatari ya mwanaume kupata Virusi vya Ukimwi (VVU) anapofanya ngono kwa kutumia uume wake. Hatari ya kupata Virusi vya Ukimwi (VVU) kutokana na ngono ya njia ya haja kubwa haitapunguzwa.
Tohara ya Hiari ya Kimatibabu kwa Mwanaume kwa kawaida imekuwa ikilenga wanaume wanaoshiriki ngono na wanawake kwa sababu tuna ushahidi zaidi kwamba Tohara ya Hiari ya Kimatibabu kwa Mwanaume hupunguza hatari ya maambukizi kutoka kwa mwanamke kwenda kwa mwanamume. Lakini zaidi ya yote wahudumu wa afya wanasema kuwa njia hii salama na ya gharama nafuu ya kuzuia VVU inapaswa kuwalenga wanaume ambao wanafanya ngono na wanaume pia.
Je, tohara kwa mwanaume ina manufaa gani kwa wanawake?
Wanawake hunufaika na Tohara ya Hiari ya Kimatibabu kwa Mwanaume kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Ikiwa wanaume wengi katika jamii wametahiriwa na wana uwezekano mdogo wa kupata VVU, hii inamaanisha pia kuwa wana uwezekano mdogo wa kuwaambukiza wenzi wao wa kike Virusi vya VVU. Wanaume waliotahiriwa wana uwezekano mdogo wa kupata magonjwa mengine ya zinaa, kama vile Virusi vya Magonjwa ya Ngono (HPV), virusi vinavyosababisha saratani ya mlango wa kizazi. Hii tena ina faida kubwa sana kwa wanawake na wasichana, kwani hupunguza uwezekano wa wao kupata saratani ya mlango wa kizazi, saratani inayotokea sana na inayoweza kuwa mbaya sana kwa wanawake.
Baadhi ya tafiti zimeonyesha kuwa kuwashirikisha wanawake na wasichana katika uhamasishaji wa Tohara ya Hiari ya Kimatibabu kwa Mwanaume kunaweza kuwahimiza wanaume kutahiriwa. Wenzi wengi wa kike huunga mkono sana Tohara ya Hiari ya Kimatibabu kwa Mwanaume kwani wanaelewa faida yake kwao na wanaiona kama ishara kwamba wenzi wao wa kiume wanatunza afya zao wote.
Ukeketaji ni nini? Kwa nini ni hatari?
Ukeketaji ni kitendo hatari. Hauna faida yoyote ya kiafya kwa wanawake na unaweza kusababisha shida kubwa za kiafya katika maisha yote ya mwanamke.
Kuna aina tofauti za ukeketaji, ambazo zote zinahusisha aina fulani ya kukata na kuondoa sehemu za labia, kinembe na kupunguza ufungukaji wa uke. Hakuna faida za uzuiaji wa VVU inayotokana na taratibu hizi na zinaweza kusababisha hatari kubwa ya maambukizi ya VVU. Pia, ukeketaji unaweza kusababisha maumivu makali, kiwewe cha kisaikolojia na matatizo endelevu ya kiafya ikiwa ni pamoja na matatizo ya ngono, wakati wa kujifungua na hedhi.
Ikiwa wewe au mtu mwingine ana wasiwasi kuhusu ukeketaji, zungumza na mfanyakazi wa huduma ya afya au mtu unayemwamini.