Je, VVU vimetokana na nini?
Kama ilivyo kwa virusi vya aina nyingine yoyote, VVU vilianza kwa wanyama na vikaambukizwa kwa wanadamu. Kwa VVU, virusi hivi vilitokea kwa sokwe na tumbili weusi wa aina ya mangabey na kusambazwa kwa binadamu. Sokwe na tumbili weusi wa aina ya mangabey hupata virusi vinavyofanana na VVU ambavyo vinaitwa SIV. Kuna aina fulani ya virusi hivi, viitwavyo SIVcpv, ambavyo vinalingana kabisa na VVU. Kwa kufahamu hili, inamaanisha kwamba tunaweza kusema kuwa VVU vilitoka kwa sokwe na tumbili walioathiriwa na SIVcpv. Mabadiliko madogo kwenye DNA ya SIV yalifanya virusi hivi kuweza kuambukizwa kutoka kwa tumbili na sokwe hadi kwa binadamu. Inawezekana kuwa binadamu wa kwanza walipata virusi hivi kwa kula nyama ya sokwe au tumbili walioambukizwa SIV au kwa kugusa damu yao kwenye vidonda walivyopata walipokuwa wakiwinda. Kuna dhana nyingi potofu kuhusiana na chanzo cha VVU, huku watu wakidai kuwa VVU vilitengenezwa maabarani na wanasayansi au ni adhabu kutoka kwa Mungu, dhana hizi si za kweli.
Virusi ni nini?
Virusi ni aina ya 'kijidudu', kinachoweza kukufanya upate ugonjwa. Ni vidogo mno, huwezi kuviona bila msaada wa hadubini yenye uwezo mkubwa. Virusi haviwezi kuishi vyenyewe. Huhitaji "vimelea" ili viendelee kuishi na kuongezeka. Kwa VVU, virusi hivi vinaweza tu kuishi katika mwili wa binadamu. Katika hali zote virusi huishi kwa kuvamia 'kiumbe' mwingine (hii ni pamoja na mimea, wanyama na binadamu, kimsingi viumbe vyovyote hai). Mara vinapovamia kiumbe mwingine vinaingia katika seli husika. Vikishaingia vinatumia mfumo wa seli hiyo kujizalisha. Virusi vingine ambavyo huenda umewahi kusikia kuvihusu ni SARS-CoV-2, virusi vya mafua, virusi vinavyosababisha malengelenge au virusi vinavyosababisha ugonjwa wa kinywa na miguu kwa binadamu na ng'ombe.