Usugu wa dawa za VVU (dawa kutofanya kazi) ni wa kawaida kwa kiasi gani?
Kadiri watu wengi wanavyoanza matibabu ya kupunguza makali ya VVU, usugu wa dawa za VVU unazidi kuwa wa kawaida. Kiwango cha usugu wa dawa hutofautiana kulingana na sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na aina ya dawa. Usugu wa Dawa zisizo za nukliasidi za kuzuia VVU visiingie katikati ya seli (NNRTIs) (kama vile efavrienz na nevirapine) ni wa kawaida zaidi kuliko usugu wa dawa mpya kama aina ya dolutegravir.
Shirika la Afya Ulimwenguni linapendekeza kwamba nchi zinapaswa kubadilisha haraka matibabu yao ya kwanza ya VVU kuwa ya aina ya dolutegravir ikiwa asilimia 10 ya watu wao wana usugu wa dawa za matibabu ya awali ya NNRTIs.
Usugu wa dawa za matibabu ya awali pia ni wa kawaida zaidi kati ya watoto wachanga ambao wanaweza kuwa na hatari ya viwango vya chini vya matibabu ya kupunguza makali ya virusi wakati wa ujauzito na wakati wa kunyonyesha.
Je! Unaweza kuwa na usugu wa dawa za VVU kabla ya kuanza kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU?
Ndiyo - ingawa usugu wa dawa unakuwa zaidi kwa watu ambao wameanza matibabu na walikuwa na shida ya kufuata utaratibu wa matibabu, inawezekana kuambukizwa VVU ambavyo tayari vimekuwa sugu. Hali hii inajulikana kama usugu wa dawa wa kuambukizwa na hutokea wakati mtu aliyekuambukiza VVU ana usugu wa dawa. Ili kuzuia VVU vyenye usugu wa dawa kusambazwa, unahitaji tu kutumia njia za kawaida za kuzuia maambukizi ikiwa ni pamoja na kutumia Vidonge vya kumeza mara kwa mara vya kuzuia VVU (PrEP), kondomu na kuwa katika hali ambapo virusi vya Ukimwi havigunduliki. Hii ni mojawapo ya sababu zinazofanya ikashauriwa kwamba watu wawili walio na VVU waendelee kutumia kondomu, ili waepuke kusambaza aina tofauti za usugu wa dawa kwa kila mmoja.
Usugu wa dawa mbalimbali ni pale ambapo kuwa sugu kwa dawa moja kunamaanisha kuwa huwezi tena kutumia dawa zingine za kupunguza makali ya virusi ambazo zinafanana. Kwa mfano, ikiwa unapata usugu wa dawa aina ya efavirenz inaweza kukufanya usiweze kutumia dawa zingine ambazo zinafanana sana kwani hazitaweza kudhibiti VVU pia.
Njia nyingine ya kupata usugu wa dawa za VVU ni ikiwa umetumia aina fulani ya matibabu ya kupunguza makali ya virusi hapo awali kisha ukaacha, kwa mfano ikiwa ulitumia dawa za kupunguza makali ya virusi wakati wa ujauzito na wakati wa kunyonyesha kwa njia ya kuzuia VVU visiambukizwe kwa mtoto kutoka kwa mama (PMTCT) lakini haukuendelea au ikiwa ulitumia Vidonge vya kumeza mara kwa mara vya kuzuia VVU au dawa zinazotumika baada ya kuwa katika hatari ya ukiwa umeshaathirika.
Ni mambo gani yanayoongeza hatari ya usugu wa dawa za VVU katika jamii?
Kwa sababu usugu wa dawa za VVU unahusishwa na uzingatiaji wa taratibu za matibabu inakuwa shida kubwa katika maeneo ambayo watu wanakabiliwa na vizuizi zaidi vya kupata matibabu na huduma. Sababu za hatari kwa ujumla zimegawanywa katika makundi matatu: sababu za mgonjwa, sababu za mpango na sababu za mfumo wa matibabu. Tunaelezea baadhi ya mifano mikuu ya kila moja hapa chini.
Sababu za mgonjwa: Usugu wa dawa za VVU unakuwa tatizo zaidi katika maeneo ambayo watu hawawezi kupata msaada wanaohitaji ili kuzingatia matibabu. Watu wana uwezekano mdogo wa kuzingatia utaratibu wa matibabu ikiwa wana uelewa duni wa VVU au manufaa ya matibabu. Pale ambapo watu wana shida zingine za kiafya kama vile mfadhaiko au matumizi ya dawa za kulevya, inaweza kufanya kuzingatia utaratibu wa matibabu kuwa ngumu zaidi na kuongeza hatari yao ya kupata usugu wa dawa.
Sababu za mpango: Mfano mzuri wa sababu ya mpango ni uhaba wa dawa. Uhaba wa dawa kwa kawaida ni matokeo ya upangaji duni, ununuzi na usimamizi wa taratibu za usambazaji (hizi ni hatua zinazohitajika kwa kliniki kununua na kupata matibabu sahihi ya kupunguza makali ya virusi). Ikiwa kliniki haziwezi kupata dawa zote wanazohitaji, watu watakosa dozi za matibabu yao na kuwafanya kuwa na uwezekano mkubwa wa kuwa sugu. Vivyo hivyo, mahali ambapo mpango hautoi upimaji wa kiwango cha virusi kwenye damu, kuna hatari zaidi ya usugu wa dawa za VVU kwani ni vigumu kwa madaktari kujua ni lini kutofanikiwa kwa matibabu kumetokea na mgonjwa anahitaji kubadili ili kuanza kutumia dawa tofauti.
Sababu za mfumo wa matibabu: Ikiwa mfumo wa mtu una changamoto zaidi, kwa mfano anatumia idadi kubwa ya vidonge kwa nyakati tofauti za siku, yuko katika hatari kubwa ya kupata usugu wa dawa. Hii ni kwa sababu tu ni vigumu kwao kufuatilia dawa wanazopaswa kutumia. Baadhi ya dawa zinaweza kuwa na 'kizuizi cha juu cha usugu'. Kwa mfano, kwa sababu ya jinsi dawa aina ya dolutegravir inavyofanya kazi, VVU vina uwezekano mdogo wa kuwa sugu dhidi yake na kuifanya iwe chaguo bora haswa kwa watu ambao wana shida ya kuzingatia utaratibu wa matibabu.